Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Mafundisho ya Kiislamu yanaeleza kuwa riziki ya kila mtu imekwishapangwa na Mwenyezi Mungu. Riziki haimaanishi tu pesa au mapato ya kifedha, bali inahusisha maisha kwa ujumla, ikiwa ni pamoja na:
1- Mahitaji ya maisha.
2- Amani ya moyo.
3- Afya njema.
4- Fursa za maendeleo.
5- Na heshima ya kijamii.
Hali ya Haramu:
Mtu hapati zaidi ya alivyopangiwa hata akitumia njia haramu. Anachofanya ni kubadilisha njia na ubora wa upatikanaji wa riziki yake - huku akiharibu baraka zake mwenyewe.
Mtume Muhammad (s.a.w.w) katika Hotuba yake ya Hijjatul Widaa’ alisema:
“Malaika wa ufunuo amenifahamisha kuwa hakuna mtu atakayeaga dunia kabla ya kutumia kikamilifu riziki yake aliyoandikiwa. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na tafuteni riziki kwa njia ya halali. Msikubali kuchelewa kwa riziki kukawafanya kuitafuta kwa njia ya haramu, kwa sababu hakika Allah amegawa riziki halali kwa waja wake - si haramu.” (Al-Kafi, Juzuu 5, uk. 80).
Maneno ya Imam Baqir (a.s):
“Kwa kila mtu, kuna riziki halali aliyopangiwa. Lakini riziki hiyo hiyo pia itamjia kwa njia ya haramu. Akiichukua kwa njia ya haramu, basi sehemu hiyo hiyo itakatwa kutoka kwenye halali yake.” (Al-Kafi, Juzuu 5, uk. 80)
Nasaha za Luqman kwa mwanawe:
“Ridhika na ugawaji wa Mwenyezi Mungu, na kaa mbali na tamaa. Mwizi anapoiba, Allah humpunguzia riziki yake, na bado huandikiwa dhambi ya wizi. Kama angesubiri, angeliipata hiyo hiyo kwa njia ya halali.” (Safinat al-Bihar, Juzuu 1, uk. 518).
Kisa cha Kihistoria kutoka kwa Imam Ali (a.s):
Imepokewa kwamba siku moja Amirul-Muuminina (amani iwe juu yake) alishuka kwenye farasi wake na kuingia Msikitini na kumkabidhi mtu mmoja farasi huyo. Mtu huyo aliiba hatamu (kamba) ya farasi na kukimbia. Baada ya Swala, Imam alitoa Dirham mbili (2) zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya ujira wa mtu huyo (kama malipo yake ya kumlinda farasi huyo), na akampa mtu mwingine (dirham hizo mbili ili) aende sokoni kununua hatamu (kamba) mpya. Mtu huyo alipofika sokoni, alikuta hatamu (kamba) ya farasi iliyoibwa ikiwa sokoni, ambapo mwizi yule alikuwa ameiuza kwa Dirham mbili. Mtu yule aliyeumwa na Imam, alinunua kamba (hatamu) ile na akarudi na kumweleza Imam kuhusu tukio hilo. Imam (as) alijibu kwa kusema: “Mja kwa kukosa subira anajinyima riziki ya halali, hali ya kuwa kupitia wizi wake hachumi chochote zaidi ya kile alichoandikiwa (alichopangiwa)". (Mizan al-Hikmah, Juzuu 4, uk. 123).
Madhara ya Riziki ya Haramu:
1. Kuharakisha Riziki kwa Njia Isiyo Sahihi
Mwizi au mla rushwa hutumia sehemu ya riziki yake mapema, lakini:
Inaharibika haraka kwa matumizi ya matibabu, woga, kesi, au majuto.
Kwa hiyo, anayepata kwa halali huishi kwa utulivu na faida halisi.
Siku ya Kiyama, mali hiyo ya haramu inapaswa kurejeshwa kwa wahusika, na thawabu ya subira ya waliodhulumiwa itakatwa kutoka kwa dhalimu.
2. Kutoweka kwa Baraka
Mali haramu haidumu, haina baraka.
Mara nyingi hutumika kwa matatizo ya kiafya, ajali, migogoro, au kuharibiwa ghafla.
3. Madhara ya Kisaikolojia na Kijamii
Mwizi au mdanganyifu huishi kwa hofu na wasiwasi wa kufichuliwa.
Hupoteza amani ya ndani na heshima mbele ya watu wake.
Hii huathiri sehemu ya kiroho ya riziki ya mtu.
4. Kupoteza Fursa za Maendeleo
Kutafuta haramu hupoteza muda, nguvu na uwezo ambao ungetumika kwa kujifunza, kazi halali au ubunifu.
Mwisho wa siku, mtu huyo hubaki nyuma kimaendeleo.
5. Kukandamizwa kwa Maisha ya Kiroho
Mali ya haramu huathiri moyo na roho ya mtu.
Huzuia madhara ya sala, dua, na mawasiliano na Mungu.
Huziba njia ya kupata rehema za Allah.
6. Kuchochea Kutokuaminiana kwa Jamii
Ueneaji wa mali haramu huondoa imani ya watu kwa haki, husababisha ukosefu wa usalama wa kiuchumi na ghasia ya kijamii.
7. Majuto ya Akhera
Mtu atakapogundua Siku ya Kiyama kwamba mali aliyopata kwa haramu ilikuwa ile ile aliyopangiwa kwa njia halali – atajuta sana.
Kama angevumilia, angepata hiyo hiyo bila dhambi wala mateso.
Natija ya Somo Hili:
Riziki yako ina “ukomo wa kimaumbile” - si nambari ya kichawi.
Unaweza kuijaza mapema kwa haramu, lakini:
1- Itakwisha haraka.
2- Itaondoa amani, baraka na heshima yako.
3- Itakuwa na malipo makali Akhera.
Au unaweza:
1- Kusubiri kwa subira.
2- Kufanya kazi kwa uhalali, ustadi na juhudi.
3- Na upate riziki ile ile (au zaidi kwa baraka) kwa heshima, utulivu, na ridhaa ya Mwenyezi Mungu.
Marejeo:
1-Al-Kafi, Juzuu 5, uk. 80
2-Al-Kafi, Juzuu 5, uk. 80
3-Safinat al-Bihar, Juzuu 1, uk. 518
4-Mizan al-Hikmah, Juzuu 4, uk. 123
Your Comment